JUMAPILI YA TANO YA KWARESIMA YA MWAKA - A

Somo  1                                                                                  Eze.  37: 12-14

Uhamisho wa Babeli ulikuwa kifo cha Taifa teule. Sababu ya mapendo yake, Mungu anaahidi kuwafufua Waisraeli, yaani kuwarudisha katika nchi takatifu. Ukombozi huo ni mfano wa ufufuko wa miili yetu siku ya mwisho.

 

Bwana Mungu asema hivi; Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburini yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu, enyi watu wangu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo, na kuyatimiza asema Bwana.

Hilo ndilo neno la Mungu.

Wimbo  wa katikati                                                               Zab.  130  (K) 7

K/ Kwa Bwana kuna fadhili,

Na kwake kuna ukombozi mwingi.

 

Ee  Bwana, toka vilindini nimekumbilia,

Bwana, usihike sauti yangu.

Masikio yako na yaisikilize

Sauti ya dua zangu.    K/

Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,

Ee Bwana, nami angesimama?

Lakini kwako kuna msamaha,

Ili Wewe uogopwe. K/

 

Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja,

Na neno lake nimelitumainia. Nafsi yangu inamngoja Bwana, Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,

Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,

Naam, walinzi waingojao asubuhi.

Ee Israeli, umtarajie Bwana.  K/

 

Maana kwa Bwana kuna fahdili,

Na kwake kuna ukombi mwingi.

Yeye atamkomboa Israeli

Na maovu yake yote.  K/

 

Somo la  2                                                            Rum. 8:8-11

Kadiri ya Paulo, shauku ya dhambi hutokana na mwili. Kumbe matendo mema yanayompendeza Mungu hutokana na Roho, yaani Roho Mtakatifu tuliyempokea katika Ubatizo. Basi tumfuate Roho ili tumpendeze Mungu, naye Roho atatufufua Yesu Kristo.

Somo katika waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Warumi.

Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho.

Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua  Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.

 

Hilo ndilo neno la Mungu.

Shangilio Yn: 11:25, 26

Mimi ndimi hou ufufuo, na uzima, asema Bwana;

Yeye aniaminiye mimi, hatakufa kabisa hata milele.

INJILI                                                             Yn. 11:1-45

Kufufuliwa kwa Lazaro ni ishara kwetu kwamba tukimsadiki na kumpenda Kristo, tunaunganika na uzima wake usiokoma ijapo miili yetu inakufa. Na katika hukumu ya mwisho hata miili yetu itapata utukufu wa uzima huo.

 

Somo katika Injili ilivyoandikwa na Yohane.

 

Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa Mariamu na Martha, dada yake. Ndiye Mariamu Yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa hawezi.

Basi wale waumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye hawezi. Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake na Lazaro. Basi aliposikia ya kwamba hawezi, alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo. Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena.

Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena? Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu. Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake.

Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha. Basi wale wanafunzi wakamwambia, Bwana, ikiwa amelala, atapona. Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amefuka. Nami nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwapo huko, ili mpate kuamini; lakini na twendeni kwake. Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, Twendeni na sisi ili tufe pamoja naye.

Basi Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne.

Na Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu, kadiri ya maili mbili hivi; na watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao.

Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Martha akamwambia, anajua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yesu akamwambia, mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiaye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? Akamwambia, Naam Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, Yule ajaye ulimwenguni.

Naye alipokwisha kusema hayo, alikwenda zake; akamwita umbu lake Mariamu faraghani, akisema, Mwalimu yupo anakuita. Naye aliposikia, aliondoka upesi, akamwendea. Na Yesu alikuwa hajafika ndani ya kijiji; lakini alikuwa akalipo pale pale alipomlaki Martha. Basi wale Wayahudi waliokuwapo na Mariamu nyumbani, wakimfariji,  walipomwona jinsi alivyoondoka upesi na kutoka, walimfuata; huku wakidhania ya kuwa anakwenda kaburini ili alie huko.

Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na kumwona, alianguka miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Basi Yesu  alipomwona analia, na wale Wayahudi walipofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake, akasema, Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame. Yesu akalia machozi. Basi Wayahudi wakasema, Angalieni jinsi alivyompenda. Bali wengine wao wakasema, Je! Huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife? Basi Yesu, hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake.Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne. Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu? Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.

Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia mfungueni, mkamwache aende zake.

Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Mariamu, na kuyaona yale aliyoyafanya, wakamwamini.

Hilo ndilo neno la Mungu.